DKT. BITEKO AOMBA SAPOTI YA WATANZANIA KWA TAIFA STARS

Serikali imewaomba wadau wa soka kuisapoti timu ya taifa 'Taifa Stars' katika maandalizi ya kujiandaa na michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani 'CHAN' yatakayofanyika Agosti mwaka huu itakayofanyika nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alipofungua Kongamano la wadau wa michezo kuelekea CHAN 2024 na AFCON 2027, linaloendelea kwenye Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Dk. Biteko alisema wadau wanapaswa kuunga mkono maandalizi ya timu ya taifa ili ijiandaee vyema na michuano hiyo.
"Wito kwa wadau wa soka na Watanzania kiujumla kuiunga mkono timu yetu ya taifa katika maandalizi ya CHAN, pamoja na kutoa rasilimali katika kuwezesha timu hiyo kipindi cha maandalizi, "alisema Dk. Biteko.
Naibu Waziri Mkuu huyo aliongezea kuwa ili timu ifanye vyema inatakiwa kusapotiwa na kuipatia hamasa kipindi inacheza.
Alisema mbali ya wadau kuinga mkono timu ya taifa, lakini watanzania wanapaswa kujitokeza uwanjani kwa wingi kwenda kuipa hamasa.
"Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi uwanjani kwa lengo la kuipa sapoti timu ya taifa ili ifanye vyema hadi kufika hatua ya fainali.
Dk. Biteko alisema michuano hiyo italeta fursa mbalimbali kwa Watanzania upande wa usafirishaji, malazi na burudani kutokana na idadi kubwa ya wageni ambao watakuja.