BMT IPO TAYARI KUSHIRIKIANA NA YOYOTE MWENYE NIA NJEMA YA USHIRIKIANO
service image
20 Jun, 2023

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amesema kuwa, Baraza lipo tayari kushirikiana na akademia yoyote, taasisi au mtu yeyote mwenye nia ya maendeleo ya michezo nchini.

"BMT ipo tayari kushirikiana pale mtakapohitaji, Serikali tunawaunga mkono sana na tunatoa wito kwa akademia nyingine wasisite kupata ushauri itasaidia kupata mawasiliano ya maeneo tofauti yenye manufaa,"alisema

Hayo ameyasema leo Juni 20, 2023 wakati akiwaaga wanafunzi wa 'Tan Warrios Sport Academy Limited' ya Mkoani Morogoro ambao wamepata mwaliko katika Chuo Kikuu cha Camerino cha nchini Italia katika programu ya kubadiliana uzoefu katika sekta ya Utamaduni, Elimu na Michezo ambayo itaanza tarehe 16 Juni hadi 03 Julai, 2023.

Aidha, Msitha amewataka kutumia vizuri nafasi waiyoipata kuwasilisha mawazo yao na kuonyesha vipaji walivyonavyo pamoja na nidhamu ili wafaidike zaidi.

"Jitahidini kuonyesha nidhamu za hali ya juu ili uonekane unaweza kuchukuliwa na klabu ukapata ajira katika timu ya taifa na ikifanya vizuri tutaondokanana kauli ya kichwa cha mwendawazimu," alisisitiza Msitha