MHE. MWINJUMA ATOA NENO KWA TAIFA STARS KUELEKEA MCHEZO DHIDI YA MOROCCO
service image
20 Mar, 2025


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amewakabidhi bendera ya Taifa timu ya Taifa Stars kabla ya mchezo wao muhimu wa kuwania kufuzu kombe la Dunia 2026 dhidi ya Morocco, Mchezo unaotarajia kuchezwa Machi 26, 2025.

Akizungumza wakati wa Iftar iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) jijini Tanga Machi 20, 2025 Mhe. Mwinjuma amesema Watanzania, wakiongozwa na mwanamichezo namba moja Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, watakuwa nyuma yao hivyo wakatangulize uzalendo ili kushinda mchezo huo.

Mhe. Mwinjuma amesema ingawa Morocco ni timu yenye sifa kubwa barani Afrika, Taifa Stars wana uwezo wa kushinda mchezo huo ikiwa watajituma na kuwa na dhamira ya kushinda. Ameongeza kuwa ushindi huo utaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

"Morocco watakuwa wachezaji 11, na sisi tutakuwa 11. Ikiwa mtaweka dhamira, uzalendo, na kufuata maelekezo ya kocha, mtashinda. Mmeshinda michezo mingi ngumu kabla, na mnaweza kufanya hivyo tena," amesema Mh. Mwinjuma.

Mhe. Mwinjuma amesema serikali inatambua umuhimu wa michezo na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akijitolea kuhakikisha kuwa fedha za kusaidia michezo zinapatikana aidha a’memshukuru Rais kwa juhudi zake za kusaidia vilabu na timu ya taifa.