DKT.GWAJIMA AWATAKA WAZAZI KUWARUHUSU WATOTO KUSHIRIKI KATIKA MICHEZO

Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Dokta Dorothy Gwajima amewataka wazazi wawaruhusu watoto wao wa kike wajitokeze kushiriki michezo kwani inajenga afya nani chanzo cha ajira.
Mhe. Gwajima ameyasema hayo leo tarehe 21 Januari, 2023 wakati akifungua mashindano ya riadha ya wanawake (Ladies First 2023) yaliyoanza kutimua vumbi kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam.
"Mashindano haya ni muhimu, wasichana wengi watapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao, Serikali ipo tayari kuimarisha na kuendeleza ushirikiano wetu na nchi ya Japani kupitia michezo, alisema.
Waziri huyo alisema ushiriki wa wanawake katika michezo mpaka sasa takwimu zinaonyesha kuwa chini ukilinganisha na wanaume.
"Ushiriki wa wanawake katika michezo ni mdogo tofauti na wanaume na hii imetokana na majukumu waliyonayo ikiweko kutopata elimu ya kutosha kuhusu michezo",alisema Waziri
Aidha amempongeza muasisi wa mashindano hayo Kanali Mstaafu Juma Ikangaa ambaye ndio ametoa wazo lake ambalo limezaa matunda ya kufanyika kwa michuano hiyo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa Leodiger Tenga alisema anawapongeza washiriki wote na kuwataka kutumia vema fursa hiyo ili kujiendeleza zaidi.
"Mashindano haya ni muhimu kwetu kwa kuwa wasichana wanapata fursa ya kuendeleza vipaji vyao katika michezo,"alisema Tenga.
Naye mwakilishi wa Taasisi ya Japan (JICA) ambao wameshirikiana na Baraza la Michezo (BMT), pamoja na Chama cha riadha Tanzania (AT) Naofumi Yamamura alisema lengo lao ni kuinua vipaji vya riadha kwa wasichana pamoja na kuendeleza mchezo wa kurusha mkuki ambao ndio umeiletea medali ya kwanza Tanzania kupitia mwanamke Teresia Dismas.
Mashindano hayo yameshirikisha wasichana kutoka Mikoa 31 ya Tanzania Bara pamoja na Visiwani vya Zanzibar ambapo wanakimbia mita 100 hadi 10,000.