DR. ABASSI AVITAKA VYAMA VYA MICHEZO KUANGALIA FURSA ZA VYAMA VYAO KIMATAIFA
service image
12 Jul, 2022

Na. Najaha Bakari - DSM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abassi amevitaka Vyama vya michezo kuangalia fursa zilizopo katika vyama vyao vya kimataifa wakati Serikali ikiendelea kutafuta rasilimali tofauti ili waende sambamba katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya michezo nchini.

Rai hiyo ameisema leo Julai 12, 2022 wakati alipokutana na Viongozi wa vyama vya michezo itayoshiriki katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola ili kujiridhisha na maandalizi yao kuelekea katika michezo hiyo inayotarajiwa kuanza tarehe 28 mwezi huu na kuhitimishwa tarehe 08 Agosti, 2022 Birmingham nchini Uingereza.



Michezo inayoiwakilisha nchi katika mashindano hayo ni pamoja na mchezo wa kuogelea, ngumi za ridhaa, wanyanyua vitu vizito kwa watu wenye ulemavu, Judo, ambapo kundi la kwanza linatarajiwa kuondoka Julai 23 wakati wachezaji wa riadha mbio ndefu wanatarajiwa kuondoka Julai 26, 2022.

Timu hizo zinatarajiwa kuagwa tarehe 20 Julai, 2022 jijini Dar es salaam, huku bendera ya Tanzania ikitarajiwa kupeperushwa tarehe 25 wakati ufunguzi wa rasmi wa mashindano hayo ukitarajiwa kufanyika tarehe 28 Julai, 2022 Birmingham nchini Uingereza.