SERIKALI KURUDISHA VIWANJA VYA MICHEZO VILIVYOVAMIWA
service image
07 Mar, 2025

Serikali imepanga kuanza zoezi la kurudisha viwanja vya michezo ambavyo vilivamiwa ili kutoa nafasi kwa michezo kuendelea.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT), Bi. Neema Msitha wakati akijibu maswali mbalimbali ya wadau wa michezo kwenye kongamano la Wadau wa Michezo Wanawake ambalo linafanyika leo Machi 07, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Aliongeza kuwa, yapo ambayo hayajatengwa basi yatengwe na baada ya hapo watatafuta wadau au wadhamini wa kuweza kuyaendeleza ili kutoa nafasi kwa watu kushiriki katika shughuli za michezo na burudani.

“Serikali itaorodhesha maeneo yote ambayo yamevamiwa baada ya hapo itashirikiana na Wizara ya Ardhi kuona namna gani vinarudishwa ili kutoa nafasi kwa michezo mbalimbali kuchezwa na kuondoa changamoto ya viwanja”, amesema Msitha.

Kongamano la Wadau wa Michezo Wanawake ambalo limeandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) linalojulikana kama Tanzanite Women Sports Festival 2025 limeshirikisha zaidi ya washiriki 200 kutoka kwenye taasisi, vyama na vituo mbalimbali vya michezo katika Mkoa wa Arusha.

Mada mbalimbali za kuelimisha Wanawake zimejadaliwa lakini pia hadithi za mafanikio kwa wanawake waliyofanya vizuri katika tasnia ya michezo Mkoani Arusha.