KASKAZINI UNGUJA BINGWA LADIES FIRST 2023
service image
22 Jan, 2023

Medali mbili za dhahabu za Winfrida Makenji za mita 100 na 200 zimeiongoza timu ya mkoa wa Kaskazini Unguja kutawazwa bingwa wa jumla kwenye mashindano ya wanawake kitaifa ya Ladies First yaliyofanyika kwa siku mbili kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Dhahabu nyingine kwa timu hiyo zilikuwa za relay ya mita 100 mara 4 ambayo Makenji aliwaongoza pia wenzake na medali ya kurusha mkuki ya Mwanaamina Hassan na ile ya mbio za mita 400 aliyoshinda Jane Maige huku mkoa huo pia ukivuna fedha moja.

Mashindano hayo yameratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la maendeleo Japan (JICA) ambao ndio wamefadhili kwa asili kubwa na yameshirikisha timu za wanawake kutoka mikoa 30 ya bara na visiwani huku Songwe ikikosa mwakilishi.

Arusha imetwaa nafasi ya pili ikishinda dhahabu nne na shaba nne, Magdalena Shauri akishinda dhahabu tatu peke yake kwenye mbio ya mita 800, 1,500 na 5000 na Jackline Sakilu akitwaa dhahabu ya mita 10,000 wakati Pwani imemaliza nafasi ya tatu ikitwaa fedha tatu na shaba moja.