MCHENGERWA:SERENGETI GIRLS IMETIMIZA NDOTO ZA WATANZANIA KUINGIA KATIKA HISTORIA YA KUSHIRIKI KOMBE LA DUNIA
service image
06 Jun, 2022

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa (Mb) amesema timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) imetimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na watanzania kwa ujumla kuingia katika historia ya kushiriki mashindano ya Dunia katika mpira wa miguu kwa wanawake.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo tarehe 6 Juni, 2022 wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/2023 ya bajeti ya wizara hiyo, ambapo amesema ni bora sasa timu nyingine za Taifa zikaiga mfano nzuri na wakizalendo ulionyeshwa na Serengeti Girls katika mpira wa miguu.

“hakika wametutoa kimasomaso kwani haikuwa kazi rahisi hata kidogo, tukumbuke kuwa wenzetu wapo katika ramani nxuri ya mchezo wa mpira wa miguu, lakini timu yetu imepambana kizalendo bila kumuogopa mpinzani wake na kutuheshimisha kama Taifa, hakika hili limetimiza ndoto ya Mhe.Rais na watanzania kuingia katika historia kushiriki mashindano ya Dunia,”alisema Mhe. Mchengerwa.

Aidha Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa serikali ilijenga matumaini na kuzalisha uzalendo kwa wachezaji wa Serengeti Girls sanjari na kuwapa ari ya kuendelea kushinda mashindano ya kimataifa na hatimaye kufuzu kombe la Dunia.

“Mheshimiwa Naibu Spika serikali ilijenga matumaini na kuzalisha uzalendo kwa wachezaji wetu,lakini pia licha ya hayo tuliwapa ari ya kuendelea kushinda mashindano ya kimataifa na hatimaye sasa tumeweza kufuzu kucheza kombe la Dunia 2022 nchini India,”alisema Mhe. Mchengerwa.