MHE.KASSIM MAJALIWA HAONGOZA HARAMBEE YA KUCHANGIA TIMU ZA TAIFA.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ameongoza Harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Timu za Taifa Serengeti Girls na Tembo Warriors ambazo zinajiandaa na mashindano ya kombe la Dunia kwa Mpira wa Miguu wanawake chini ya umri wa miaka 17 nchini India pamoja na Mpira wa Miguu kwa watu wenye Ulemavu nchini Uturuki mwezi Oktoba, 2022.
Tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Selous wa Kituo cha Mikutano Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), ambapo Mhe. Majaliwa amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza katika tukio hilo muhimu, ambalo linaleta chachu kubwa katika maendeleo ya michezo nchini.
Mhe.Majaliwa amesema pia Tanzania inayoongozwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ina matumaini ya kufanya vizuri katika mashindano hayo ya kombe la Dunia, kutokana na Ari iliyoonyeshwa na wachezaji katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Jijini Birmingham nchini Uingereza.
Jumla ya kiasi cha Fedha kilichopatikana katika Harambee hiyo ni zaidi ya Tshs.1.2 Bilioni.