MSAJILI AFANYA MAAMUZI
service image
26 Jul, 2022

Na. Najaha Bakari - DSM

Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Njombe (Njorefa)Tobias Bosco Lingalangala pamoja na Katibu Mkuu Obed Mwakasungura wamefungiwa kwa muda wa miaka miwili kujihusisha na masuala yoyote ya mpira ndani na nje chama hicho kutokana na kutokidhi vigezo vya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya Chama.

Ameyaeleza hayo leo tarehe 26 Julai, 2022 Msajili wa Vyama vya Michezo hapa nchini Riziki Majala wakati akiongea na Waandishi wa habari, alisema adhabu hiyo imetokana na viongozi hao kushindwa kuthibitisha kuwa na elimu ya sekondari kidato cha nne na kidato cha sita, ikiwa ni matakwa ya katiba ya chama hicho.

Msajili huyo alisema toleo la sasa ibara ya 29(2 )na 29( 7) ya Katiba ya Njorefa inahusu sifa za kuwa wagombea (viongozi) hususan Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, na Katibu Msaidizi.

"Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 28 cha Baraza la Michezo (BMT) sura ya 49 kikisomwa na kanuni ya 10(1) na 10(1) c ya kanuni za usajili wa vyama vya Michezo, tangazo la Serikali namba 441 ya mwaka 1999,"alisema Msajili huyo.

Alisema adhabu hizo zilianza tangu Julai 20 mwaka huu na kudai watuhumiwa hao wanaruhusiwa kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya michezo nchini.

Aliongeza kuwa adhabu hizo zimetolewa baada ya kupitia malalamiko mbalimbali ambapo alifanya uchunguzi na kubaini ukweli hivyo kuamua kuwafungia.