MSITHA ATOA WITO KWA MIKOA KUCHANGAMKIA FURSA YA KUJITANGAZA KUPITIA RIADHA WANAWAKE

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Neema Msitha ameziomba kamati za michezo za mikoa kuwezesha ushiriki wa wanariadha wa mikoa katika mashindano ya riadha kwa wanawake “Ladies First” yanayotarajiwa kuanza tarehe 21 hadi 22 mwezi Januari 2023 katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa.
Hayo ameyasema leo tarehe 19 januari, 2023 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mashindano hayo yaliyoratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa kwa kushirikiana na Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan [JICA].
“Kamati za michezo za mikoa hakikisheni mnawasafirisha washiriki wote kutoka mikoa yenu ili waweze kushiriki katika mashindano haya, lakini pia nawataka shirikisho la riadha nchini kusimamia mashindano haya kwa weledi mkubwa” alisema Msitha.
Msitha ameishukuru Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Japan [JICA] na kampuni za kijapani zinazo fanya kazi nchini Tanzania kwa ufadhili wa mashindano haya kwa mara ya nne.
“Tunaishukuru JICA kwa mchango wao mkubwa katika kudhamini mashindano haya kwa msimu wa nne sasa, ambao wamekuwa wakigharamia zaidi ya asilimia themanini (80%) malazi, chakula na gharama nyingine zote za uendeshaji wa mashindano hayo”Alisema.
Aidha, Msitha, ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutoa uwanja wa Taifa utakaotumika katika mashindano hayo huku akiwaomba wananchi waishio Jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi siku ya mashindano ili kuwapa hamasa washiriki.
Kwa upande wake mwakilishi wa JICA nchini Naofumi Yamamura amesema kuwa, lengo kuu la mashindano hayo ni kuhakikisha jamii inapata uelewa juu ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya michezo na kueleza kuwa, wataendeleza ushirikiano na Tanzania katika kukuza sekta ya michezo.
Mashindano hayo yatashirikisha wanariadha wakike takribani 186, kutoka Tanzania bara na Zanzibar yatakayohusisha mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1,500, 5,000, 10,000, 400X4 relay pamoja na kurusha Mikuki [Javelin], na yanatarajiwa kushuhudiwa na Wanafunzi takribani 1000 kutoka baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari kutoka manispaa ya Temeke