MSITHA AUTAKA UONGOZI WA RIADHA TANZANIA (AT) KUJITATHMINI NA KUWASILISHA TAARIFA MBALIMBALI ZA KIUTEKELEZAJI.
service image
20 Jan, 2023


Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Y. Msitha, ameutaka uongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (AT) kujitathmini utendaji wake kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya masuala ya kiutendaji katika Shirikisho hilo.

Msitha ametoa rai hiyo leo tarehe 20 Januari, 2023 alipoitisha kikao cha kamati Tendaji ya AT pamoja na baadhi ya watendaji wa BMT kilichofanyika katika moja ya kumbi za uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo pia amesema viongozi wanapaswa kuzingatia misingi ya Utawala bora ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa ya miaka miwili (2) ya mapato na matumizi ya AT katika kipindi cha mwezi mmoja.

“kwa kweli Baraza haliridhishwi na utendaji uliopo katika Shirikisho la Riadha, hivyo ni vyema nyinyi viongozi mkajitathmini utendaji kazi wenu, mnapaswa kuzingatia sana misingi ya utawala bora kwa kutekeleza yale mnayotakiwa kutekeleza kiuadilifu,” amesema Msitha.

Aidha Msitha pia amesisitiza uongozi wa AT kuwasilisha mpango mkakati wa Shirikisho kwa mwaka mzima kwa kuzingatia mambo muhimu ambayo yamekuwa hayafanyiki mara kwa mara kama vile mashindano ya riadha Taifa pamoja na kuwasimamia wajumbe wa kanda kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kwa upande wake makamu wa rais wa AT William Kallaghe ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na BMT katika kipindi cha muda mfupi ikiwemo kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi ya miaka miwili, mpango mkakati wa AT pamoja na kufanyika kwa mashindano ya riadha Taifa.