MSITHA AWATAKA MAKATIBU WA KAMATI ZA MICHEZO ZA MIKOA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA MUJIBU WA SHERIA

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka Makatibu wa Kamati za michezo za Mikoa ambao ni maafisa michezo katika ngazi za Mikoa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya michezo kwa mujibu wa sheria ya BMT na sheria za nchi.
Rai hiyo ameitoa leo Disemba 01, 2022 katika kikao kazi cha BMT na Maafisa michezo baada majadiliano ya kina kuhusu namna bora ya kuendesha mashindano mbalimbali kwa mustakabali wa maendeleo ya michezo nchini na kimataifa.
Msitha ameongeza kwa kuwataka kufanya maandalizi ya wachezaji katika ngazi zao watakaoshiriki katika mashindano yaliyopo mbele yao ikiwemo mashindano ya Mbio za wanawake (Ladies First) ambayo yanayarajiwa kufanyika mwezi Januari, pamoja na mashindano ya Taifa (Taifa Cup) yanayotarajiwa kufanyika mwezi Februari 2023.
Aidha, ameongeza kwa kuwataka pia kuhakikisha mbio tofauti zinazoendeshwa katika ngazi zao na ngazi za halmashauri zinasajiliwa na kuwa na kibali cha kuyaendesha kutoka baraza ili kuwa salama linapotokea tatizo lolote lakini pia kuyaendesha kwa kufuata sheria.