MSITHA AZIPONGEZA KAMPUNI ZA BIMA KUISAIDIA SERIKALI KUENDELEZA MICHEZO NCHINI.

Na.Najaha Bakari - DSM
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amezipongeza kampuni za bima nchini zikiwakilishwa na Demeter na Willmars kuisaidia Serikali katika ajenda yake ya kulisukuma gurudumu la maendeleo ya michezo.
Rai hiyo ameitoa leo Julai 04, 2022 Ofisi kwake kabla ya kupokea vifaa vya mchezo wa kabaddi kutoka kwa kampuni hizo za bima wakiwakilisha na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa kampuni ya Demeter Victoria Lukuwi.
"Kuwekeza kwenye michezo kuna mrejesho mkubwa kwa kuwa unaifikia nguvu kazi kwa kiwango kikubwa ambao ni vijana nani wengi, kufanya hivyo unaisaidia serikali na kujenga mahusiano mazuri,"alisema Msitha.
Vifaa hivyo vimepokelewa ikiwa ni maandalizi ya wanamichezo wa timu ya taifa ya mchezo wa Kabaddi ambao wanajiandaa kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika ya mchezo huo ambayo yanatarajiwa kuanza Julai 22 hadi 29, 2022 Cairo nchini Misri.
Hata hivyo Msitha amewataka Viongozi wa mchezo wa Kabbadi nchini kuwafikishia vifaa hivyo walengwa ili wajiamini na kuiwakilisha nchi kwa ushindi katika mashindano hayo.
"Viongozi boresheni mahusiano, jijengeeni kuaminika na makampuni kwa kufikisha vile wanavyotoa vya walengwa,"alisisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa timu hiyo ya taifa ya mchezo wa kabaddi Anna Msulwa ameishukuru Serikali kupitia BMT kwa nguvu kubwa kuendeleza michezo nchini.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na jezi pea 90, viatu vya kuchezea pea 48, raba pea 48, traksuti 60, skin tight za kuchezea 60, mabegi ya kuwekea vifaa 60, 6 0 - vikinga mikono (long sleev) na "nee guard" 60.