MSITHA: NENDENNI KAIWEKENI NCHI KATIKA ULIMWENGU WA MICHEZO

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Mtendaji Mkuu Bi. Neema Msitha limewataka wachezaji wanaokwenda kwenye mashindano ya Afrika kwa upande wa mpira wa wavu kuhakikishe wanapambana waweze kupata matokeo mazuri.
Mashindano ya Mataifa ya Afrika ya Mpira wa wavu kwa wanaume yamepangwa kuanza kutimua vumbi Septemba 3 hadi 14, 2023 mwaka huu nchini Misri.
Timu ya Tanzania yenye wachezaji 12 inawakilishwa na wachezaji kutoka klabu za ndani na nje ya nchi ambayo inatarajia kuondoka tarehe 02 Septemba kuelekea nchini Misri .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba Mosi, 2023 wakati akiwakabidhi bendera ya Taifa Bi. Neema Msitha, amesema kuwa lengo ni kuhakikisha Tanzania inaonekana katika ulimwengu wa michezo.
Ameendelea kwa kuwataka wachezaji kuonesha ushindani na kutambue kuwa wameenda kushindana na si kushiriki.
"Matamanio ya serikali ni kuona timu inakwenda kushindana na matumaini yetu makubwa kutoka kwenu tunataka kusikia katika timu mbili zitakazofuzu kwenda kushiriki mashindano ya Dunia na Tanzania tuwepo," alisema Msitha.
Naye Naibu katibu Mkuu wa Chama Cha Mpira wa wavu Tanzania (TAVA) Shukuru Ally, amesema kuwa, wamejiandaa kwenda kupambana na wachezaji wana ari ya kuhakikisha wanaenda kupata walichokusudia,"alisema.