MSITHA: TUMIENI VYOMBO VYA HABARI KUJIBRAND
service image
26 Jun, 2022



Na. Najaha Bakari - DSM

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha amewataka Viongozi wa Vyama vya Michezo kutumia vyombo vya habari kujitangaza ili kupata wafadhili mbalimbali wa kuwekeza katika michezo yao, ili kuendesha shughuli zao kwa kujiamini ikiwemo mashindano.

Rai hiyo ameitoa leo tarehe 25 Juni, 2022 wakati akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya michezo Dkt. Hassan Abbas kufungua mashindano ya mchezo wa Vishale ya Afrika Mashariki yaliyoanza jana Juni 24 katika ukumbi wa Jeshi wa fukwe ya Msasani, ambayo yatafikia tamati kesho tarehe 26 Juni, 2022.

Aidha, Msitha amewashukuru wanachama wa mchezo huo wa Afrika kwa ushirikiano wao katika kuendesha mashindano tofauti katika ukanda huo lakini pia kuamua mwaka huu yafanyike nchini Tanzania.

Mashindano hayo yameshirikisha nchi tatu akiwemo mwenyeji Tanzania, Kenya na Uganda katika michezo ya timu (Inter State) na Michezo ya mtu mmoja mmoja (Singles).