NAIBU KATIBU MKUU YAKUBU ATAKA UWAJIBIKAJI KWA MAAFISA MICHEZO
service image
01 Dec, 2022

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu amewataka maafisa michezo kuwajibika ipasavyo kila mtu katika eneo lake ili kuendeleza juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya michezo.

Yakub ameyasema hayo leo tarehe 01 Desemba, 2022 wakati akifunga kikao kazi cha Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Makatibu wa kamati za michezo za Mikoa kilicholenga maendeleo ya michezo nchini.

"Mafanikio katika sekta ya michezo, sisi tuliopo humu ndani tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha kuwa tunasimamia michezo katika ngazi za chini ili tuweze kuibua na kuendeleza vipaji kwa wingi"

Ameongeza kuwa makatibu hao hawanabudi kuwa na mipango madhubuti ya kusimamia michezo katika ngazi zote pamoja na kuwa na program maalum ya kuibua na kuendeleza vipaji.

"Kusimamia Utawala bora katika Vyama vya Michezo vya Mikoa, kuhakikisha taasisi za michezo zilizopo zinasajiiwa, kutambuliwa na kusimamia uhai wa Vyama hivyo "

Aidha, amewataka waendelee kushirikiana na wadau ikiwemo Makampuni ili kupata udhamini wa shughuli za michezo katika ngazi zao pamoja na ukuzizisimamia Halmashauri ili ziweze kutekeleza shughuli za michezo.

"Ni matumaini yangu kuwa kama kila mtu atajitoa na kutekeleza wajibu wake ipasavyo Tanzania itapiga hatua kubwa sana ya kuendeleza michezo kwa kuwa tunayo hazina kubwa ya vipaji vya michezo"

Naibu Katibu Mkuu Yakubu amewahakikishia Makatibu hao kuwa , changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao kuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo (WUSM) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI wataendelea kuzisimamia na kuzipatia ufumbuzi.