UONGOZI MPYA SHIMIVUTA WATAKIWA KUONGEZA WANACHAMA WAPYA
service image
27 Oct, 2023

Viongozi wapya wa Shirikisho la Michezo ya Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (SHIMIVUTA) wametakiwa kuongeza wanachama wapya pamoja na kuhakikisha wanasajiliwa na kulipa ada kwa mujibu wa Sheria na kanuni za Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Hayo yamesemwa leo Oktoba 27, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Nicholus Mihayo kutoka BMT baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa viongozi hao uliofanyika Jijini Tanga, huku akiwataka kufanya kazi kwa pamoja ili kuliinua shirikisho hilo.

Aidha, Mihayo ameongeza kwa kuwataka kutumia vyombo vya habari katika matukio yao ili kuonekana na kuwavuta wawekezaji watakaosaidia maendeleo ya Shirikisho hilo.

Kwa niaba ya Viongozi hao, Rais Mpya ya Shimivuta Juhudi Samu ameihakikishia Kamati ya uchaguzi kutekeleza maagizo waliyotoa huku akiwashukuru wajumbe wa mkutano wa uchaguzi pamoja na kuwaomba ushirikiano na kuwatuma ili kulipeleka pazuri shirikisho hilo.

Juhudi Samu ndiye Rais mpya wa Shimivuta aliyeibuka kwa kura zote 47 za ndiyo, Makamu wa Rais Elifadhili Mpehongwa aliyepita kwa kura 43 za ndiyo ambao hawakuwa na upinzani, huku nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa na wagombea wawili Ashrafu Athumani mshindi kwa kura 36 dhidi ya mpinzani wake Augustino Saqware aliyepata kura 10.

Wengine ni nafasi ya Katibu Msaidizi iliyochukuliwa na Faraja Mbagale kwa kura 45, mweka hazina Fidea Chale aliyepata kura zote 47 wakati nafasi ya wajumbe wanne (4) kwa mujibu wa Katiba ya Shimivuta imechukuliwa na Joshua Senguo kwa kura 45, Mwanahamisi Mkwizu, Silvanus Ntirumolekwa na Adventina Msiba walioshinda kwa kura 46 kila mmoja.