PONGEZI KWA UONGOZI WA TaBSA KUFANYA VIZURI KATIKA UTENDAJI WAKE
service image
27 Jan, 2023

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha ameupongeza uongozi wa Chama cha Baseball na Softball Tanzania (TaBSA) kwa kuendelea kufanya vizuri katika utendaji wa shughuli zake kwa kufuata misingi ya Utawala Bora.

Msitha ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2023 alipotembelewa ofisini kwake na Katibu wa TaBSA Alpherio Nchimbi aliyeambatana na Mkurugenzi wa Shirika la Baseball la Caribbean kutoka nchini Marekani Bw. Mario Signorello ambaye amekuja nchini kwa ajili ya kuendesha kliniki ya wachezaji wa Baseball kupitia mradi wa mchezo huo Barani Afrika.

"Kwanza kabisa niupongeze uongozi wa TaBSA umekuwa ukifanya kazi vizuri sana, hivyo Bw. Signorello nikuhakikishie kuwa unafanya kazi na mtu sahihi kabisa ni kiongozi ambaye amekuwa akiwajibika na kukiongoza chama vizuri, hivyo nadhani mradi huu utafanyika vizuri hapa nchini na kupata mchezaji sahihi katika kliniki utakayoendesha kupitia mradi wa Baseball Afrika ambao ndio umekuja nchini kwa mara ya kwanza", amesema Msitha.

Kwa upande wake Katibu wa TaBSA Nchimbi amesema mradi wa Baseball Afrika utakuwa na manufaa makubwa kwa wachezaji wa Tanzania kwani kupitia kliniki ya baseball itakayoendeshwa katika shule ya Sekondari Azania tarehe 28 Januari, 2023,itatoa mchezaji mmoja ambaye atapata ufadhili wa kwenda kusoma katika chuo ya Florida Memorial kilichopo nchini Marekani.