SERIKALI KUJENGA UWANJA MKUBWA ZAIDI (SPORTS AND ARTS ARENA) BARANI AFRIKA

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, imesema ipo katika hatua za kurekebisha na kujenga miundombinu ya michezo nchini, ikiwemo ujenzi wa uwanja mkubwa wa kisasa kwa ajili ya michezo mbalimbali (Sports and Arts Arena) ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji elfu kumi na sita (16,000).
Hayo yamezungumza leo tarehe 30 Aprili, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu alipokuwa anafunga mashindano ya Kanda ya Tano ya mchezo wa Judo yaliyofanyika katika uwanja wa ndani wa Don Bosco Upanga jijini Dar es Salaam.
“sisi kama serikali tunatambua kuwa moja ya jukumu letu kubwa ni kuandaa, miundombinu sahihi kabisa kwa ajili ya mashindano ya mbalimbali,na niwaambie kwamba tupo katika hatua za kujenga uwanja wa kisasa (Sports and Arts Arena) ambao utajengwa Kawe Dar es Salaam, tunaendelea na taratibu mbalimbali ikiwemo kutafuta zabuni, na uwanja huu utakuwa ndio mkubwa zaidi kwa sababu vile viwili vilivyopo Senegal na Kigali nchini Rwanda vinauwezo wa kuingiza watu elfu kumi (10,000) na elfu 12,000 lakini wa kwetu utaingiza watu elfu kumi na sita (16,000).
Aidha Yakubu amesema kuwa Mheshimiwa Rais amejitoa sana katika kuimarisha michezo nchini ikiwemo kuongeza Bajeti ya kugharamia timu za Taifa, kwani bajeti hiyo imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka milioni mia mbili sabini (270,000,000) hadi Bilioni Moja na Nusu (1,500,000,000).
Lakini pia amesisitiza uongozi wa mchezo wa Judo Tanzania kuendelea kuutangaza mchezo pamoja na kutoa hamasa ili kuongeza ushiriki wa wanawake zaidi katika mchezo huo.