Serikali kuunga mkono TADA kuwa mwanachama wa Dunia
service image
25 Jun, 2022

Na. Najaha Bakari

Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha, amewaeleza Viongozi wa TADA kuwa Serikali itashirikiana nao kuhakikisha chama cha Darts Tanzania (TADA) kinakuwa mwanachama wa Dunia.

Kauli hiyo ameitoa jana Juni 25, 2022 wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Afrika Mashariki ya Darts yanayoendelea kwenye viwanja vya fukwe ya Msasani, Jijini Dar Es Salaam.

Amesema kuwa hiyo ni fursa ya kuhakikisha mchezo huo unafika mbali na kuwa sehemu ya ajira kwa kuchezwa kwa malipo kama ilivyo nchi za Ulaya.

"Tukiwa ni walezi wa vyama vya michezo tumechukua maelekezo ya mwakilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha tunakuwa wanachama wa Shirikisho la Dunia ," amesema Neema.

Ameongeza kwa kuwataka kuwapa kipaumbele vijana kucheza mchezo huo sambama na watoto kushiriki kikamilifu ili iwe fursa ya ajira kwao.

Naye Mwakilishi wa Jumuiya Afrika Mashariki David Alex Tabaso, amezishauri nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha zinajiunga na uanachama wa Shirikisho la Dunia.

Alitaja nchi hizo kuwa, ni pamoja na Kenya, Zanzibar, Rwanda, Sudani Kusini na Tanzania kuwa wanachama kama ilivyo Uganda pekee ambayo ndio mwanachama tayari.

Wakati huo huo mashindano ya Afrika Mashariki ya Darts yanatarajiwa kuhitimishwa leo tarehe 26 Juni, 2022 kwa washindi wa mchezaji mmoja mmoja, wawili wawili na timu kutangazwa .

@@@