SERIKALI YA TANZANIA YAISHUKURU SERIKALI YA INDIA KUIUNGA MKONO MCHEZO WA KABADDI.

Na. Najaha Bakari
Serikali ya Tanzania kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeishukuru Serikali ya India kuendelea kuisaidia katika kukipa nguvu chama cha mchezo wa kabaddi nchini kuendeleza mchezo huo na kuiwakilisha nchi katika mashindano tofauti ya kimataifa.
Shukrani hiyo imetolewa leo Julai 15 na
Afisa Michezo wa Baraza la Michezo Taifa (BMT) Allen Alex wakati alipoambatana na Kaimu Balozi wa India nchini kushuhudia mazoezi ya timu za taifa za mchezo huo ambazo ziko kambini kujiandaa kuelekea katika mashindano ya Afrika nchini Misri.
Allen alisema mchezo huo asili yake ni India na kudai wameweza kuwaletea mwalimu ambaye anaifundisha timu hiyo ambapo kwa upande wa Afrika timu hiyo ipo katika ngazi ya pili (Ranking).
"Tunafurahi kuona wanazidi kuisaidia timu yetu pamoja na kumleta mtaalamu anayewafundisha, matarajio yetu tunaamini itakwenda kufanya vizuri,"alisema Allen.
Aliongeza kuwa, katika mashindano hayo zinatakiwa timu tatu ambazo zitashinda zitaende kushiriki mashindano hayo ya Dunia.
Naye Kaimu Balozi wa India Manoj B. Verma amesema kuwa, lengo la mashindano hayo ni kwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini India.
Akizungumza na wachezaji hao leo Julai 15 wakiwa mazoezini balozi huyo aliwataka wachezaji hao kwenda kufanya vizuri kwenye mashindano hayo waweze kurudi na medali ya ushindi nyumbani Tanzania.
"Ninaomba muende mkaiwakilishe vizuri timu yenu ya Tanzania tutaendelea kushirikiana na nyie bega Kwa bega kuhakikisha mnakwenda kufanya vizuri,"alisema.
Alisema anayofuraha kuona mchezo wa kabbadi Tanzania unachezwa na unafanya vizuri, hivyo wataendelea kuusapoti mchezo huo.