SERIKALI YATARAJIA KUPATA MIPIRA 64,000 KUTOKA FIFA
service image
29 Aug, 2023

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema Serikali itapokea mipira 64,000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ili kuibua vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu nchini.

Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema hayo Agosti 28, 2023 Mkoani Njombe wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

"Mipira hiyo inatolewa na Shirikisho la Mipira wa Miguu nchini (FIFA) na itasambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ili kusaidia kuibuliwa kwa vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu" amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha amesema, mipira hiyo itatolewa na FIFA kupitia programu ya 'FIFA for Schools programme' ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia BMT, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) ambao wameingia mkataba na FIFA kutekeleza programu hiyo.