TLGU WATAKIWA KUWEKEZA ZAIDI KWA WATOTO NA VIJANA WANAOCHEZA MCHEZO WA GOFU.
service image
25 Mar, 2023

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limewataka viongozi wapya wa Chama cha Gofu Wanawake (TLGU) kuwekeza zaidi katika kukuza vipaji vya watoto na vijana wanaocheza mchezo wa Gofu, ili kuwa na timu bora ya Taifa itakayoleta ushindani zaidi katika mashindano ya kimataifa.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 25 Machi, 2023 na Afisa Michezo wa BMT Benson Chacha, mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi wa viongozi wa TLGU uliofanyika katika viwanja vya Gofu Lugalo jijini Dar es Salaam.

“Timu ya Taifa ya Gofu wanawake imekuwa na wachezaji walewale siku zote, hivyo ni vyema viongozi mlioingia madarakani kuna haja kubwa ya kuwekeza kwa watoto na vijana wanaocheza Gofu, ili tuweze kuwa na timu bora hapo baadae hawa wachezaji wengine watakastaafu kucheza mchezo huu,”alisema Chacha.

Kwa upande wake Rais wa TLGU Queen Siraki ameishukuru kamati ya uchaguzi kwa kusimamia uchaguzi huo kwa haki na uwazi, pamoja na kuahidi kuendeleza zaidi mazuri yote yaliyofanywa na uongozi uliopita, ili kuendelea kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

“kwa niaba ya viongozi wenzangu tuliochaguliwa, kwanza kabisa tunaishukuru kamati ya uchaguzi kwa kusimamia uchaguzi huu kwa haki na uwazi, lakini pia niahidi kwamba tutaendeleza zaidi mazuri yote yaliyofanywa na uongozi uliopita, ili tuendelee kufanya vizuri kitaifa na kimataifa,”alisema Siraki.

Viongozi wengine waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Ayne Magombe - Makamu wa Rais, Yasmin Chali - Katibu wa Heshima, Joyce Ndyetabura - Mhazini na Hawa Wanyeche - Katibu wa Mashindano.