TPBRC YAHIMIZWA KUREKEBISHA KANUNI ZA UENDESHAJI.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Afisa Maendeleo ya Michezo na mwenye dawati la Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBRC), Allen Alex ameitaka Kamati ya Utendaji ya Kamisheni hiyo kurekebisha kanuni zake za uendeshaji kwa maslahi mapana ya kamisheni hiyo na maendeleo ya mchezo wa ngumi hizo kwa ujumla.
Hayo ameyasema leo tarehe 6 Februari 2023, katika kikao na viongozi wa juu wa kamisheni hiyo kilichofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
Aidha Allen amewahimiza viongozi hao juu ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Kamisheni hiyo ambao haujafanyika kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Vilevile, Allen amewashauri viongozi wa TPBRC kuwa, wanapaswa kuongeza ushirikiano baina yao na BMT, na kuongeza juhudi katika uhamasishaji wa upatikanaji wa wanachama wengi zaidi kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa chama hicho.