TPC WATAKIWA KUTUMIA VIFAA WALIVYOPOKEA KWA KAZI ILIYOKUSUDIWA

Na.Najaha Bakari - DSM
Baraza la Michezo la Taifa ( BMT) limetoa maelekezo kwa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) wakasimamie na wakavitumie vifaa kwa malengo yaliyokusudiwa. Vifaa vya ofisi vilivyotolewa na ubalozi wa china nchini Tanzania vyenye thamani ya shilingi milioni 20 zikiwemo kompyuta 6 (desktop), laptop 6, mashine ya kopi, na projetor.
Wito huo umetolewa leo tarehe 13 Julai, 2022 na Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo katika Ofisi za Baraza Jijini Dar es salaam.
Alisema kuwa BMT haitasita kufuatilia na kusimamia kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kama ilivyokusudiwa.
"Tunashukuru wenzetu wa China kwa moyo walioufanya kusaidia vifaa vya ofisi kwa watu wa Kamati ya Paralimpiki ninaamini ofisi yao itakamilika na watafanya kazi zao kwa bidii,"alisema Neema.
Mtendaji huyo aliipongeza Kamati hiyo kutokana na kuamua kukaa chini na kuomba msaada huo kutoka China na kuvitaka vyama vingine viige mfano huo.
"Nitoe changamoto kwa vyama, Mashirikisho na Kamati kuiga mfano huo na kuuliza wamefanyaje Ili kuweza kupata misaada hiyo kwakuwa Serikali tunasimamia wengi lakini hatuwezi kuwafikia wote," alisema.
Naye Balozi wa China Chen Mingjian, alisema ameamua kukabidhi vifaa hivyo kutokana na ukaribu mzuri uliopo kati ya nchi ya China na Tanzania hususani kwenye suala zima la Michezo.
"Baada ya kupata maombi kutoka kwa watu wa Paralimpiki hatukusita kuwasaidia kwa kuwa tunatambua umuhimu wa michezo hasa kwa watu wenye ulemavu,"alisema Mingjian.
Kwa upande wa Rais wa Kamati ya Paralimpiki Tanzania (TPC) Tuma Dandi alisema anashukuru kupokea vifaa hivyo ambavyo walikuwa wanavihitaji Kwa muda mrefu.