TWA WAITA WADHAMINI

Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo wa WUSHU Tanzania (TWA) Mwarami Mitete, ameyaomba makampuni mbalimbali kuwadhamini katika mashindano ya taifa yanayotarajiwa kufanyika kwa siku mbili Novemba 26 na 27 mwaka huu katika Uwanja wa ndani wa Mkapa Jijini Dar es salaam.
Mitete, ameyasema hayo leo tarehe 17 Novemba, 2022 wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuwataarifu wadau kuhusu mashindano hayo yanayotarajia kushirikisha vilabu 60 nchi nzima huku washiriki wakiwa wanaume na wanawake lakini pia itahusisha watoto.
"Mashindano haya yamedhaminiwa na ubalozi wa China pamoja na kampuni ya Crost Limited ambao lengo lao ni kuona mchezo wa Wushu unaendelea kuibua vipaji na unafanya vizuri zaidi hapa nchini,"alisema Mitete.
Naye Kocha wa mchezo wa Wushu, Master Ramadhan Mshana alisema anawaomba wachezaji kutoka vilabu shiriki kujiandaa vizuri kabla ya kuja kushiriki mashindano haya kwani hii itakuwa fursa kwao kupata nafasi ya kuitwa kwenye timu ya taifa.
Naye Afisa Masoko wa kampuni ya Crost Limited, Rehema Kamara alisema lengo la kuudhamini mchezo wa Wushu ni kusaidia kuukuza mchezo huo na kuinua vipaji vipya kwenye mchezo huo.