VIONGOZI WAPYA OBFT WAAGIZWA KUSIMAMIA UTAWALA BORA

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Halima Bushiri, amewataka viongozi wapya wa Shirikisho la ngumi za wazi Tanzania (OBFT) kuzingatia utawala bora pamoja na uwajibikaji kwenye majukumu yao.
Hayo ameyasema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa Shirikisho hilo uliofanyika leo tarehe 12 Februari, 2023 katika ukumbi Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam.
"Hakikisheni katika kipindi chenu cha utawala mnasimamia utawala bora, uwazi, uwajibikaji na kuwashirikisha wanachama wenu ili kuliimarisha Shirikisho,"alisema.
Naye mkuu wa dawati la michezo ya ngumi zikiwemo za wazi Allen Alex, amewaagiza viongozi hao kuhakikisha shirikisho hilo linapata ofisi yake, linakuwa na akaunti, pia waongeze juhudi kwenye usajili wa wanachama, pamoja na kuimarisha mipango mikakati ya kuliingizia kipato Shirikisho hilo ili liweze kuimarika kwa kujiendesha lenyewe.
Kwa upande wake, Afisa michezo Nicholas Mihayo amelitaka Shirikisho kuongeza utendaji yakinifu na kuhakikisha wanasuluhisha migogoro yao kwa njia halali ikiwezekana kuimaliza kabisa migogoro ndani ya Shirikisho hilo.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Lukelo Anderson Willilo aliyeshinda nafasi ya Rais kwa kura 19 dhidi ya Samwel Christopher Sumwa aliyepata kura 3 kutoka kwa wapiga kura halali 22. Huku nafasi ya Makamu wa Rais ikichukuliwa na Nasoro Abbasi Makau mgombea pekee kwa kura 15 za ndiyo pamoja na Katibu Mkuu Makore Mashaga aliyepata kura 20 za ndiyo.
Wengine ni nafasi na mweka hazina iliyokwenda kwa Rwegasira Samson mgombea pekee aliyepata kura 12 za ndiyo, na kwa upande wa wajumbe Kamati ya walimu ni Mafuru Magoti aliyepata kura 19, Kamati ya Ufundi ni Michael Mugeni kwa kura 21 na Kamati ya Mashindano na Vifaa ni Ruger Kahwa aliyepata kura 16.
Asha George Mwanamke pekee aliyegombea katika uchaguzi huo katika kamati ya wanawake na Vijana ameibuka kidedea kwa kura zote 22 za ndiyo, Iddy Rugundana kamati ya maendeleo ya mikoa na taasisi za umma ameibuka na kura 17 na Samwel Kapungu kamati ya AOB, APB na WSB aliyepata kura zote 22 za ndiyo.