WACHEZAJI WA GOFU WATAKIWA KUWA NA NIDHAMU KAMBINI.

Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Apansia Lema amewataka wachezaji wa Timu ya Taifa ya mchezo wa Gofu wanawake, kuwa na nidhamu na kujituma pindi wawapo kambini wakati wakijiandaa na mashindano yajayo ya Gofu kwa wanawake Afrika yanayotaraji kuanza Septemba 3 2022, katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
Lema ameyasema hayo leo tarehe 25 Agosti, 2022 alipowatembelea na kuongea wachezaji hao walioweka kambi katika klabu ya Gymkhana.
Kwa upande wake rais wa Chama cha Gofu wanawake Sophia Virgo amesema uongozi wake umejipanga kuhakikisha timu inafanya vizuri licha ya changamoto ya kukosa udhamini wa kutosha kuiandaa timu.
Naye Nahodha wa timu ya wanawake Hawa Wanyeche amesema kuwa wako tayari kupambania Taifa katika mashindano hayo makubwa Afrika na kuhakikisha kuwa kombe linabakia nyumbani.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo yatakayoshirikisha nchi 24 ikiwemo Kenya,Zimbabwe Afrika Kusini, Gabon, Zambia n.k.